Kwa Mwenyehisa Mpendwa

Matokeo ya Benki hii kwa kiwango kikubwa ni sawa na hali ilivyokuwa kanda ya Afrika Mashariki ambapo mataifa mengi yalianza kuimarika tena kiuchumi na kuwa na nguvu, licha ya mazingira ya kibiashara kuwa magumu. Matokeo haya ya kuridhisha ni ishara ya muundo bora wa kibiashara ambao tumekuwa tukiutumia kuwahudumia wateja wetu. Tuna wafanyakazi wenye motisha, Bodi yenye maono na tunapokea uungwaji mkono kutoka kwako, mwenyehisa mpendwa. Unaposoma ripoti hii, utapata kwa kina hali halisi ya matokeo yetu ya kifedha.

Niruhusu nikudokezee mambo makuu kuhusu matokeo haya. Tunashikilia asilimia 15% ya amana, ambazo ni pesa zilizowekwa na wateja kwenye benki sokoni. Tunashikilia pia 17% ya mikopo eneo hili. Baadhi hueleza hili kuwa somo la msingi katika sekta ya benki. Kwa kuangalia mambo ya msingi, tunasalia kuwa benki yenye nguvu Zaidi eneo hili.

Tunavutia kwa wingi na kuweka pesa za wateja, jambo ambalo linatuwezesha kutoa mikopo ya bei nafuu kwa wateja pia. Si ajabu kwa hivyo kwamba mapato yetu yalisalia kuwa ya juu. Kwa mapato tulipata 20% ya mapato yoyote sokoni, na ukuaji wa 24%.
Tukiuchambua mwaka 2018, sekta hii ilikumbana na changamoto nyingi.

Viwango vya riba tunavyoruhusiwa kutoza vilipunguzwa mara mbili katika mwaka huu. Hii iliathiri sehemu muhimu ya mapato ya benki hii, ambayo ni mapato kutoka kwa riba.

Mazingira magumu ya kibiashara pia yaliathiri biashara katika sekta nyingine, ambazo pengine mwenyewe unafanyia kazi au una hisa. Kwa mtazamo wa mfadhili, tulishuhudia biashara kadha zikiwezwa chini ya mrasimu katika mwaka huo na nyingine zikatoa tahadhari ya kupungua pakubwa kwa faida. Hii inatilia mkazo kauli yangu ya awali kwamba mazingira ya kibiashara yalikuwa magumu kweli. Lakini licha ya changamoto hizi, nina furaha kwamba wafanyakazi wetu katika maeneo tunayoendesha biashara walitafuta njia na namna ya kuwasaidia wateja wetu. Inaridhisha kwamba haikuwa masikitiko kote, tulishuhudia biashara zikijikwamua na hata kukua kwa kiwango sawa au hata zaidi ya ukuaji wa uchumi.

Shughuli za kibiashara

Mmenipa jukumu, mimi na kundi langu, kufanikisha matokeo mazuri na kuimarisha uwezo wa Benki hii kuhakikisha tunasalia kileleni. Ukitazama jinsi matokeo yetu yalivyokuwa mwaka huo, utaona kwamba faida yetu baada ya kulipa ushuru ilipanda na kufikia KShs 23.9 bilioni. Gharama zilidhibitiwa vyema na ziliongezeka kwa kiwango kilichokuwa chini ya kiwango cha mfumko. Kiwango cha mikopo ambayo hailipwi nacho kilishuka na kufikia 6.9% ukilinganisha na kiwango cha wastani katika sekta hii cha 12%. Ili kuharakisha kujikwamua kwa ubora wa mikopo tuliyoitoa, tulianzisha kitengo maalum cha kuangazia mali yetu ambacho kitashughulikia mikopo mikubwa ambayo hailipwi kwa sasa na ambayo inahitaji njia tofauti kuishughulikia. Kwa jumla, na jambo ambalo naamini ni la maana sana, hili lilituwezesha kuongeza mgawo wa faida kwa kila hisa kwa 17% hadi KShs 3.50.

Kama biashara, tumegundua kwamba njia pekee ya kuendelea kuwepo katika biashara ambayo bidhaa zinafanana ni kwa kuangazia huduma bora kwa wateja. Wateja wetu ndio nguzo ambayo imetuwezesha kuwa Benki kubwa zaidi katika kanda hii. Ndio maana tumeamua ni lazima tuelekeze upya juhudi zetu katika kuhakikisha kwamba tunawahifadhi wateja wetu, na pia kuwavutia wengine zaidi, kwa kutoa huduma ambazo zinakidhi mahitaji yao. Lengo letu ni kuwaelekeza makusudi wateja wetu hadi kwenye maeneo yenye ukuaji, kuwezesha biashara kukua na mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki kunawiri kiuchumi. Mwishowe, tutawasaidia watu kutimiza matamanio yao na ndoto zao za kifedha na uwekezaji.

Biashara ya kanda na mtazamo wa kimataifa

Sehemu kubwa ya wenyehisa wetu tumekuwa nao kwa miongo mingi na wanakumbuka tulipofungua kampuni yetu tanzu ya kwanza Tanzania mwaka 1997. Tangu wakati huo, kampuni zetu tanzu katika mataifa ya kanda hii zimekuwa sehemu kubwa ya mpango wetu. Tulijumuisha Jumuiya ya Afrika Mashariki Sudan na Ethiopia kwenye mkakati wetu mkuu hizi majuzi. Ethiopia inaendana vyema na ndoto zetu za siku za usoni, ukizingatia ukuaji wake kiuchumi na idadi kubwa ya watu. Tunafuatilia kwa karibu mazungumzo yetu na wasimamizi na mamlaka za serikali kuhusu uwezekano wa kufanyia marekebisho sheria kuruhusu benki za nje kuhudumu nchini humo.

Kufikia Desemba 2018, biashara katika kampuni zetu tanzu ilikua kwa zaidi ya 65% mwaka baada ya mwaka. Lakini licha ya ukuaji huu mkubwa, mchango wake ulisalia kuwa chini ya 10% kwa mapato ya jumla ya Kampuni. Sababu za mchango huu wa chini hivi zinafahamika na wasimamizi wanaziangazia katika ngazi ya nchi na kwa uelekezi wa Mkurugenzi wa Biashara za Kanda wa Kampuni ambaye wajibu wake mkuu ni kuhakikisha mchango huu unafikia 20% kufikia 2022.

Tunatambua kwamba matukio nje ya nchi na kimataifa yataathiri biashara zetu. Biashara zetu katika mataifa mengine kadha hii binafsi zimeathirika na changamoto nyingi miongoni mwake mizozo ya kisiasa na misukosuko ya kiuchumi. Kwa pamoja, uchumi wa mataifa huathiriwa pia na matukio katika mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi. Mfano ni vita vya kibiashara vya hivi majuzi kati ya Marekani na Uchina, na kujiondoa kwa Uingereza kutoka kwa Umoja wa Ulaya Kukabili uhalifu wa kifedha Kampuni ya KCB inatambua mchango mkubwa unaotekelezwa na mfumo wa kifedha katika kukabiliana na uhalifu wa kifedha. Kama benki yenye mtazamo wa kimataifa, tutajijengea sifa za kukabiliana na utakatishaji na ulanguzi wa fedha kwa kufuata maadili ya kuwafahamu vyema wateja wetu.

Tunaendelea kuimarisha uwezo wetu wa kuwakinga wateja wetu na sisi wenyewe dhidi ya uhalifu wa kifedha. Tunaamini hili litakwua na manufaa kwa wateja wetu pamoja na kuimarisha sifa zetu na uhusiano wetu na washirika wengine kimataifa, zikiwemo benki nyingine.
Licha ya juhudi zetu, Benki ya KCB Kenya iliadhibiwa na serikali chini ya mfumo wa kisheria wa Kukabiliana na Utakatishaji wa Fedha / Kukabiliana na Ufadhili wa Ugaidi (AML/ CFT). Tumechukua hatua zaidi kuwakumbusha tena wafanyakazi wetu wote kuhusu kanuni na taratibu zinazofaa kufuatwa kukitokea shughuli za kibiashara za kutiliwa shaka. Tunaunga mkono juhudi hizi zenye lengo la kuimarisha na kulinda sekta ya kifedha katika kanda hii.

Uendelevu

Benki yako ilikuwa miongoni mwa kampuni za kwanza kanda hii kukumbatia uendelevu kwenye shughuli zake, mwongo mmoja uliopita. Mtazamo wetu unaangazia kuhakikisha mustakabali bora kwa vizazi vijavyo; hatuwezi kubadilisha msimamo huu. Kama sehemu ya mchango wetu, tunatekeleza mchango muhimu na kuwa katika mstari wa mbele katika Mkakati wa Maadili ya Kifedha kuhusu utoaji huduma za Benki kwa Uwajibikaji. Huu ni mkakati wa Umoja wa Mataifa unaolenga kuhakikisha benki zinaangazia uendelevu katika shughuli zake. Tunafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba tunapunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani. Katika ripoti hii, tumeeleza kwa kina baadhi ya shughuli tunazozifanya na matokeo yake katika kuhakikisha uendelevu.

Ili kuendeleza ajenda yetu ya uendelevu, tunaendelea kuwashirikisha wateja wetu na kampuni zinazotuuzia bidhaa na huduma kuhusu haja ya kuendesha shughuli kwa njia endelevu.

Miongoni mwa mengine, tuliandaa warsha ya kuwahamasisha wanaotuuzia bidhaa na huduma na kuwafunza kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Tutaendelea kusaidia kampuni na biashara nyingine kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani na kuhamia katika ‘uchumi wa kijani’. Tutafadhili uvumbuzi wa teknolojia za kuhifadhi mazingira, kuhamasisha kampuni kuhudumu katika njia zinazosaidia jamii, kuheshimu haki za kibinadamu na kuangazia maendeleo yanayowajumuisha wote.
Ninaamini kwamba tunaongoza katika juhudi hizi.

Kama sehemu ya ajenda hii, KCB imekumbatia viwango vya ubora vya Mazingira, Jamii na Usimamizi (ESG) na kwa ushirikiano na washirika mbalimbali tumetoa mafunzo na vyeti kwa wafanyakazi 250 wa utoaji mikopo kuhusu utekelezaji wa maadili hayo, kuhakikisha wanatumia ESG katika kutathmini zaidi ya 90% ya mikopo. Huwa tunachapisha Ripoti ya Uendelevu kando kila mwaka, ambapo huwa tunaeleza kwa kina miradi yetu na matokeo yake.

Watu wanaofanikisha mambo

Ili kuendesha Benki hii, tumewaajiri wafanyakazi zaidi 6,200 kutoka nchi na asili mbalimbali. Ni kupitia
kungi hili ambapo tunaweza kuandikisha matokeo ya kuridhisha mwaka baada ya mwaka. Mkakati wetu wa kuwaangazia wafanyakazi umesalia na kusaidia pakubwa katika kukumbatia kwa teknolojia mpya. Kuhusu kuongeza ujuzi, mafunzo yetu hutolewa darasani na mtandaoni. Mwaka 2019, ni hitaji kwa wafanyakazi wote, nikiwemo, kumaliza kozi za mtandaoni kuhusu uendelevu, afya na usalama, maadili, kukabiliana na utakatishaji wa fedha, uendelevu wa biashara, usalama wa teknolojia ya habari na mawasiliano, na mafumzo mengine muhimu kwa kazi ya kila mfanyakazi na kwa kujiendeleza mwenyewe.

Kuna hitaji kubwa la uwezo mpya katika utengenezaji na usimamizi wa mifumo mpya ya teknolojia na hazina data kwa sasa. Ushindani katika kupata wataalamu wachache waliopo ni wa juu mno lakini tumefanikiwa kuwafihadhi wataalamu ambao wameandaa na kudumisha bidhaa na huduma bora zinazotumiwa na wateja wetu. Kadhalika, tumewekeza katika watu wa kulinda mifumo na mtandao wetu dhidi ya wahalifu wa mtandaoni.

Usalama wa mifumo na mtandao wetu ni muhimu sana katika kulinda fedha za wateja wetu. Tutalipa kipaumbele suala hili kwani tukio moja la uvamizi linaweza likaharibu matunda ya juhudi za miaka mingi.

Katika mwaka huo, kulikuwa na mabadiliko kadha kwenye wasimamizi wa ngazi ya juu yaliyoendana na mkakati wetu na hatua zinazopigwa na benki hii. Katika ngazi ya wasimamizi wakuu, tulimteua Mkurugenzi wa Kampuni wa Biashara za Kanda na pia Mkurugenzi wa Huduma za Benki za Wateja Wakubwa. Katika mwaka 2018, wafanyakazi 155 walipandishwa ngazi na kupewa majukumu mapya baada ya kudhihirisha uwezo wa kufanya makujumu zaidi na hamu ya kuendeleza mkakati wa Kampuni.

Shughuli ya kuwatafuta watu wa kujaza nafasi nyingine muhimu inatarajiwa kukamilishwa mwaka huu. Hizi ni pamoja na Mkurugenzi wa Wafanyakazi (nafasi iliyoshikiliwa na Mkurugenzi wa Kampuni wa Biashara za Kanda), Mkurugenzi wa Shughuli, MD (Meneja Mkurugenzi) wa Wakala wa Bima wa KCB, MD wa Benki ya KCB Bank Sudan Kusini na MD wa Benki ya KCB Uganda.

Uhusiano na wafanyakazi umekuwa muhimu sana katika kuhakikisha wana motisha na pia wanajitolea kazini. Ni kwa kutilia maanani jambo hili ambapo kesi katika mahakama ya leba iliyokuwepo tangu 2017 ilitatuliwa. Tuliongeza pia mikutano yetu na wafanyakazi hadi 142% ambapo kulikuwa na mikutano 130 na wafanyakazi, ikiwemo vikao vya mameneja wa matawi, majukwaa ya wanawake na wanaume walio uongozini, mabaraza na hafla ya kuimarisha uhusiano baina ya wafanyakazi wenyewe. Tulihitimisha mwaka kwa sherehe ya Tuzo za Simba ya kuwatuza wafanyakazi bora kote katika kanda hii.

Mkakati wa kutumia teknolojia

Mojawapo ya mambo ninayoyathamini sana ni utoaji wa huduma za benki kupitia njia rahisi na inayofikiwa na wengi. Nimefuatilia na mimi ni muungaji mkono wa matumizi ya teknolojia katika kufanikisha maendeleo endelevu, kupunguza pengo katika uwezo wa kiuchumi na kijamii na kuhakikisha kila mtu anafikia fursa za kumsaidia kuboresha maisha yake, hasa kupitia huduma za kifedha. Ndio maana tumefanya “dijitali kwanza na kwa haraka” kuwa sehemu ya mkakati wetu wa kurahisisha kupatikana kwa mikopo na kuhakikisha wateja wanafurahia utoaji huduma wetu.

Mwaka 2018, mafanikio yetu makuu yalikuwa uzinduzi wa mfumo mpya wa utoaji huduma kidijitali. Hili limetusaidia kupanua na kurahisisha upatikanaji wa mikopo huku tukiboresha ubora wa utoaji huduma kwa wateja. Aidha, tumepunguza gharama ya utoaji huduma kwa wateja wetu na hivyo kuongeza mapato kwako wewe, mwenyehisa wetu.

Kupitia kutumia teknolojia, tumetumia mfumo wa ngazi mbalimbali katika kuamua gharama ya huduma na pia kuimarisha alama za uwezo wa kukopeshwa za wateja wetu. Hili limewezekana kupitia kutumia teknolojia na wanasayansi wa data kukadiria alama za uwezo wa kukopeshwa na kuweka vipimo kwa kuzingatia tabia na uwezo wa wateja. Kiwango chetu cha wastani cha ukopeshaji kinakaribia KShs 5,000 lakini tuna wateja wenye uwezo wa kukopa zaidi ya KShs 100,000 – ishara ya tofauti zilizopo baina ya wateja wetu na uwezo wa mfumo wetu. Kipimo cha juu kimedhihirisha hamu ya kukopa miongoni mwa wamiliki wa biashara, na kutoa fursa ya kutoa alama za uwezo wa kampuni mbalimbali kama ilivyofanyika kwa wateja binafsi.

Huu ni mwanzo tu wa msururu wa uvumbuzi unaotarajiwa kurahisisha mambo. Katika kusaidia ukuaji wa biashara kupitia muundo huu, leo hii tunakabiliwa na changamoto la washindani wetu ambao hawakuwepo zamani. Wateja wetu wana mambo mengi kando ya hatari ya kawaida ambayo awali ilitumiwa kukadiria gharama ya mkopo. Uwazi katika kukadiria gharama ya mkopo na alama za uwezo wa kukopeshwa za mtu binafsi ni muhimu siku hizi sawa na kasi ambayo mkopo unatolewa. Kwa hivyo, hatulegezi juhudi zetu katika uvumbuzi.

Kutokana na mabadiliko yanayoshuhudiwa siku hizi, uwezekano wa mapato siku za usoni kutoka kwa biashara za sasa pekee ni mdogo mno. Ujuzi wetu na kasi katika kutangaza huduma zetu kupitia njia mbadala ndio utakaotupa mapato ya kutuwezesha kutimiza lengo letu la kupata 40% ya mapato ya jumla kutoka kwa shughuli zisizohusiana na riba.

Fursa kuu mbele yetu

Serikali ya Kenya imetaja nguzo nne kuu za kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi ambazo ni: makao na nyumba za bei nafuu, huduma bora ya afya kwa wote, kujitosheleza kwa chakula, na viwanda. Ingawa bado tumekuwa tukichangia kwa kiasi Fulani katika kila moja ya nguzo hizi, tunatafakari jinsi ya kutekeleza mchango muhimu zaidi katika kutimiza malengo haya. Watumiaji wa bidhaa, Kilimo / Mboga na Matunda, viwanda na biashara kwa siku zijazo vitakuwa vichocheo vikuu vya ukuaji wa uchumi kanda hii, kupitia Zaidi kampuni ndogo na za wastani. Katika mataifa yote tunayofanyia biashara, mkakati wetu umewekwa mahsusi kusaidia ndoto za kiuchumi za taifa
husika. Tumejitolea na tunajiweka sawa kukumbatia ushirika na wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa kusaidia sekta muhimu na wajasiriamali ikiwemo kupitia matumizi ya teknolojia kutatua masuala ya gharama ya mikopo na utoaji wa alama za uwezo wa kukopeshwa.

Fahari yetu imesalia kuwa hatua ambazo huduma yetu ya kukopesha kupitia simu imepiga. Tunalenga kutoa mikopo ya zaidi ya KShs 100B kote nchini, na kuna fursa ya kueneza huduma hii kanda yote. Isitoshe, tutaongeza uwezo wa huduma hii kufanikisha malipo.
Kampuni hii imechukua hatua jasiri katika kuimarisha thamani kwa wenyehisa kupitia pendekezo la kuhamishwa kwa umiliki wa baadhi ya mali ya Benki ya Imperial (IR) na pia pendekezo la kununua Benki ya National ya Kenya (NBK). Matunda ya hatua hizi mbili yatajivuniwa kwa miaka mingi ijayo kupitia nguvu inayotokana na kuunganishwa kwa fedha zilizowekwa na wateja benki, kuweza kutoa mikopo kwa gharama nafuu na uwezo wa kupata mapato kutoka kwa shughuli za kibiashara za wateja watakaoongezeka.

Baada ya kuangazia mafanikio makuu, changamoto na mipango tuliyonayo, jambo la muhimu zaidi bado ni wafanyakazi wetu kutumia rasilimali tulizo nazo kutoa huduma na bidhaa bora kwa wateja. Nilipata fursa ya kukutana na wafanyakazi na wateja wengi, ambayo ni sehemu ya kazi yangu: Ningependa kuwashukuru wafanyakazi wetu wote na wateja kwa kuendelea kufanya kazi nasi.
Nathamini sana uhusiano wetu na asanteni sana kwa kuamua kuitumia benki yetu.

Joshua Oigara, CBS

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kundi na Mkurugenzi
Mkuu