Taarifa ya Mwenyekiti wa Kundi

Kampuni ya KCB lilitimiza ahadi zake za 2018 kutokana na mkakati endelevu wa ukopeshaji pamoja na uboreshaji wa huduma za kidijitali. Utathmini wangu wa matokeo ya Kampuni ni kwamba ni ya kuridhisha na yanalingana vyema na bajeti kwa jumla.
Ufanisi huu ulipatikana licha ya changamoto kadha kama vile athari za kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2017 nchini Kenya. Uchaguzi huo uliathiri kwa jumla mazingira ya uendeshaji biashara. Pia, kulitokea mabadiliko ya kisheria. Mambo haya mawili yaliathiri kwa kiasi fulani ukuaji wa biashara yetu.

Licha ya haya, ukuaji wa kiuchumi uliendelea kwa kiwango cha kuridhisha, ambapo kulikuwa pato la jumla la taifa lilikuwa 6% katika mataifa ambayo huwa tunaendesha shughuli zetu. Biashara yetu Kenya Ilichangia kwa kiwango kikubwa faida yetu. Kampuni zetu tanzu katika mataifa hayo mengine pamoja na KCB Capital na Wakala wa Bima wa KCB zote zilichangia mapato ya Kampuni kwa njia ya kuridhisha. Lengo sasa ni kuhakikisha kampuni tanzu zinachangia zaidi ya 20 % ya faida ya Kampuni kufikia 2020, kutoka kwa kiwango cha sasa cha 6%. Kutokana na kulipatia kipaumbele suala hili na umuhimu wake, Bodi iliamua kumteua afisa mtendaji mwenye uzoefu mwingi, Paul Russo, kuwa Mkurugenzi wa Biashara za Kanda wa Kampuni hii kuanzia Januari 1, 2019. Amepewa jukumu la kuongoza ajenda hii kuanzia ngazi ya juu kabisa ya Kampuni kuhakikisha kampuni tanzu zinafanya kazi kwa njia bora zaidi na zimefungamanishwa na maono ya Kampuni.

Siku zijazo, tunatarajia kampuni tanzu zivune matunda ya uwekezaji ya kiwango sawa au hata bora zaidi kuliko biashara yetu Kenya. Bodi hata hivyo inatambua kwamba kila kampuni tanzu hutenda kazi katika mazingira tofauti ya kibiashara. Mabadiliko yoyote ya kimikakati yanayohitajika katika kila kampuni tanzu ni lazima yazingatie hilo pamoja na kufuata masharti na sheria katika nchi husika.

Kama sehemu ya mkakati wetu katika kanda hii, tunafurahia kwamba kuna kuongezeka kwa kasi katika kufanya huru sekta muhimu za kiuchumi nchini Ethiopia. Kampuni yetu imekuwa na afisi ya uwakilishi ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa miaka mitatu sasa Addis Ababa.

Ni matumaini yetu kwamba tumepata ufahamu wa kutosha wa soko nchini humo na hivyo basi tupo katika nafasi nzuri ya kuingia katika soko hilo lililo na watu zaidi ya milioni 100 fursa hiyo itakapotokea.Bodi inatambua mchango unaotekelezwa na KCB katika kanda hii unaoendelea kuongezeka. Uhusiano wetu na serikali, wateja, na jamii katika maeneo tunayofanyia kazi pamoja na wafanyakazi wetu ni sehemu muhimu ya mkakati wetu katika kutekeleza vyema wajibu tuliopewa na wenyehisa.

Tunatekeleza hili kupitia:
– Mabilioni ya pesa yametolewa kwa wateja kuwasaidia kukuza biashara zao na kuboresha maisha yao
– Kukumbatiwa na kuzingatiwa kikamilifu kwa viwango vya ubora na matakwa ya kisheria.
– Kutoa fursa kwa wateja kuweka akiba na kuwekeza pesa zao za ziada katika uwekezaji unaozalisha riba
– Kutoa ajira kwa wafanyakazi 6,220.

– Kuwekeza pesa na kutekeleza miradi yenye lengo la kutatua shida mbalimbali na kuboresha hali ya maisha katika jamii.

Mustakabali

Sekta ya benki nchini Kenya imeshuhudia kuungana kwa benki kadha miaka ya karibuni. Hata hivyo, ndipo sekta hii ibaki kuwa thabiti na yenye ushindani, kunahitajika kasi zaidi katika kuungana huku kwa benki. Kenya ina benki nyingi kupita kiasi ukilinganisha na mataifa mengine ya kiwango sawa kiuchumi barani kwa mfano Nigeria na Afrika Kusini. Katika kanda hii, Rwanda na Tanzania zimedhihirisha kuwepo kwa uwezo mkubwa wa mapato zaidi kutoka kwa sekta ya kifedha. Kampuni ya KCB inaendelea kutafuta fursa za kukuza zaidi sekta ya kifedha.

Mabadiliko ya kidijitali

Mabadiliko ya kidijitali yamebadilisha sana uchumi na kuathiri pia biashara yetu. Kama Kampuni,
tumeendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia kutoa huduma za kifedha, maarufu
kama Fintech, na matunda yake yameonekana.

Leo hii, tupo miongoni mwa kampuni zinazoongoza kwa kutoa mikopo kwa wingi kupitia mfumo wa dijitali. Kama bodi, tutazidi kuangazia kutoa mwongozo wa kisera kwa wasimamizi wa kampuni kuhakikisha tunasalia wepesi wa kuchukua hatua
katika ulimwengu huu wa kidijitali unaobadilika kila uchao.

Usimamizi wa Kampuni

Bodi inatambua kwamba tunapaswa kuendelea kuimarisha na kuboresha juhudi zetu katika utathmini na pia kuzingatia hatari mbalimbali.
Mahitaji ya kisheria ya Kukabiliana na Utakatishaji wa Fedha (AML) na Mfahamu Mteja Wako (KYC) yana umuhimu sana kwa sekta ya benki. Tuna miongozo thabiti sana ya AML na KYC ambayo huwa macho kila wakati na hutoa tahadhari mapema na kuhakikisha hatua zifaazo zinachukuliwa.
Tunatambua madhara ambayo udhaifu katika AML/KYC unaweza kusababishia kampuni yetu, pamoja na madhara mengine kwa sekta hii kwa jumla. Tumejitolea kutimiza matarajio ya mamlaka zinazosimamia sekta hii na kulinda na kutetea maslahi ya wenyehisa wetu, wateja, wafanyakazi na jamii katika mataifa ambayo tunafanyia kazi. Ili kuunga mkono juhudi hizi, tumefanya mabadiliko makubwa kwenye muundo wa bodi, na tukabadilisha idadi ya kamati za bodi kutoka sita hadi tano. Aidha, tumefanya kazi kwa pamoja na wasimamizi wa Kundi la KCB kuimarisha utathmini na uwasilishaji wa taarifa kwa bodi.
Tuna imani kwamba mabadiliko haya yataisaidia bodi kusalia kuwa makini zaidi katika kuangazia masuala ya umuhimu mkubwa zaidi kwa kampuni. Tulifanyia pia mabadiliko bodi zetu mbalimbali katika kanda ili kuleta mitazamo mipya huku tukiendelea kufaidi kutokana na uzoefu wa wanachama ambao bado wamekuwa wakihudumu. Wanachama wapya wa bodi wanatuletea uwezo mbalimbali ukiwemo utaalamu katika huduma za kifedha, usimamizi wa hatari, teknolojia, usimamizi wa vipaji, fedha na uhasibu, utoaji huduma za hisani kwa jamii na masuala ya kisheria. Nina furaha kuwajulisha kwamba katika kipindi hiki cha mpito, bodi imeendelea kuzingatia kujumuishwa kwa watu wa asili mbalimbali na kwa kufuata kanuni na maadili kwa viwango vya kimataifa na kwa kuheshimu sheria za wafanyakazi katika kanda hii.

Uendelevu

Tunatambua kwamba wenyehisa wetu wameweka imani yao katika Kampuni ya KCB. Tunaangazia kusimamia kampuni hii kutimiza malengo ya muda mrefu ya kampuni hii. Muhimu zaidi, tunatambua kwamba tunaweza tu kufanikiwa na kupata matokeo bora iwapo tutazingatia uendelevu katika biashara zetu. Lengo letu ni lazima liwe zaidi ya kutengeneza faida. Ni lazima tuzingatie pia nguzo tatu za maendeleo ambazo ni uchumi, jamii na mazingira.

KCB imekuwepo kwa zaidi ya miaka 120. Tunatumai tutakuwepo kwa miaka mingi. Ndipo tuweze kutimiza hili, ni lazima tuweke mikakati itakayohakikisha benki hii inaendelea kuwepo, na kunaendesha shughuli zetu tukizingatia maslahi ya jamii na uhifadhi wa mazingira.
Tunakusudia kuendelea kukopesha wateja kwa uadilifu, kupunguza mchango wetu katika uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani, kuzingatia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kutekeleza mchango muhimu katika mstari wa mbele kama mmojawapo wa wadau muhimu katika kanda hii wa mpango wa UNEP wa Mkakati wa Maadili ya Kifedha kuhusu utoaji huduma za Benki kwa Uwajibikaji. Kupitia KCB 2Jiajiri –mpango wetu wa kuwawezesha vijana na ujasiriamali – tumedhihirisha kwamba tunaweza kufanikisha mazingira bora ya kuwawezesha vijana kuwa wajasiriamali wanaofanikiwa.

Nguzo nne kuu

Serikali ya Kenya imetaja nguzo nne kuu ambazo itaangazia katika maendeleo ya taifa kwa miaka ijayo: huduma bora ya afya kwa wote, makao na nyumba za bei nafuu, viwanda na chakula. Kundi la KCB kwa miaka mingi limekuwa likichangia juhudi zake katika nguzo hizi kwa njia moja au nyingine. Lakini sasa tunaona fursa kuu. Serikali za mataifa mengine pia zina malengo yake ya ukuaji. Tutaendelea kuzindua mikakati ya kusaidia juhudi hizo.

Mustakabali

Tunatarajia ukuaji halisi na kutokea kwa fursa mpya mwaka 2019 kutokana na kufufuliwa kwa imani ya wawekezaji na kujikwamua kwa mataifa ya kanda hii kiuchumi. Sekta ya benki inatarajiwa kukua sambamba na ukuaji wa kiuchumi na kwa hivyo, tuna matumaini makubwa kwamba tutaendeleza ukuaji wa kuridhisha mwaka huu.

Kama Bodi, tunatambua juhudi muhimu sana zinazotekelezwa na wasimamizi katika kuhakikisha kwamba benki hii inasalia kuwa nguzo muhimu katika maendeleo katika nchi zinazohudumu. Tunatambua bidii yao. Wateja wetu na wenye hisa nao wametupa usaidizi usio na kifani na tunawashukuru pia. Ningependa pia kuwashukuru wanachama wenzangu kwenye bodi kwa uongozi na ushauri wao bora ambao umehakikisha Kampuni ya KCB inasalia kuwa benki inayoongoza katika kanda hii. Hata hivyo, hatuwezi kulegeza juhudi zetu. Bado kuna kazi zaidi ya kufanywa kutimiza lengo letu la kuwa kampuni ya thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja katika kipindi cha miaka miwili hadi tatu ijayo.

Andrew Wambari Kairu
Mwenyekiti wa Kundi